Watu watano wamelazwa katika hospitali ya Mama Lucy hapa jijini Nairobi baada ya kuumia wakati polisi walikua wakifyatua risasi katika kivuko cha reli cha Total eneo la Dandora. Mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Kamkunji Francis Kamau alisema polisi walikuwa wakilinda doria wakati walipogundua wizi wa kimabavu uliokuwa ukiendelea. Polisi walifyatua risasi walipokuwa wakikabiliana na wezi.
Kulingana na ripoti ya polisi, simu nne zilipatikana katika eneo la mkasa, moja kati ya simu hizo ilitambuliwa na mwathiriwa wa wizi na kuandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Dandora. Kati ya wale walioumia wakati wa sarakasi hizo ni abiria waliokuwa wakisubiri kuabiri gari.
Wakaazi wa eneo hilo wameeleza hofu na wasiwasi kuwa huenda polisi waliwapiga risasi wale wasio na hatia. Kamanda wa polisi wa eneo la Dandora alidai kuwa mshukiwa mmoja alikamatwa na yupo chini ya uangalizi wa polisi katika hospitali ya Mama Lucy akiendelea kupata matibabu akiwa anaauguza majeraha ya risasi.