Connect with us

Habari

Ujenzi wa Barabara ya Ngong-Lang’ata Walaumiwa Kwa vifo vya 4 Kibra

Published

on

Eneo la Mkasa katika wadi ya Lindi ambako watu wanne walipoteza maisha yao

Watu 4 wameangamia kutokana na mafuriko katika eneo la Lindi mtaani Kibra. Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa Alhamisi 13, Mei 2021 ilisababisha mafuriko hayo ambayo yalisababisha  mamia ya wenyeji kukosa usingizi wakijaribu kuzuia maji kuingia manyumbani mwao.

Kati ya wanne walioangamia walikuwemo waendeshaji bodaboda waliokuwa wakiwavukisha watu waliokwama upande mmoja wa daraja la Kibera South wakitaka kuvuka.

“Waliosombwa ni rafiki zetu tunawajua vizuri, walikuwa kwa shuguli zao za kutafuta” alisema Bw.  Ray Osuthe, mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

Mamia ya wakazi wanaoishi karibu na eneo hilo vile vile wanakadiria hasara  baada ya maji kuingia manyumbani mwao. Mmoja wa wakaazi kwa jina Mary anasema hakuweza kuokoa chochote kwani maji yalufurika kupita kiwango cha kawaida.

“Maji yaliingia mpaka karibu kwa paa sasa nimepoteza karibu kila kitu, hatukulala kabisa usiku. Tunalaumu daraja hili. Waliojenga  hawakuwafikiria watu wanaoishi hapa. Walijenga daraja ndogo sana hata maji hayawezi kupita vizuri.” Mary alisema

Vijana wenye hamaki walivamia eneo la ujenzi wa daraja mkabala na kituo cha afya cha  Kibera South, wakabomoa sehemu ya ua la mabati linalozingira eneo la kuweka mashine za kazi. Walilaumu ujenzi wa daraja hilo wanalosema lilipelekea vifo vya wenzao.

“Hili daraja lilijengwa vibaya, haifai kujenga daraja ambalo maji yanapita juu ya barabara badala ya chini. Sasa tumewapoteza wenzetu kwa sekunde chache tu kwa sababu ya daraja ambalo limejengwa ovyo “. Mmoja wa wakazi mwenye hamaki alisema.

Vijana wametishia kulibomoa daraja hilo ikiwa wanaojenga barabara hiyo inayotarajiwa kuungasha barabara za Ngong na Langata hawatarekebisha hali hiyo. Baadhi yao walisikika wakisema maji yakipungua wangelibomoa daraja hilo. Wakazi pia wamelalamikia kujikokota kwa ujenzi wa barabara hiyo

Baadhi ya mashirika ya kusaidia jamii yalikuwepo kwenye eneo la mkasa wakirekodi matukio.

Bw. Paschal Kipkemboi,  mratibu wa shirika la Kounkuey Design Initiative,  KDI, linalowasaidia wakazi wa mtaa wa Kibra kupokea taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kujiandaa kwa uwezekano wa kutokea kwa majanga anasema zaidi ya familia mia moja zimeathirika kando na wale waliopoteza maisha. “najua mamia ya wakazi wameathirika kwa njia moja ama nyingine, nyumba zao zimefurika na wamepata hasara kubwa. Lakini familia nne nazo zimepoteza wapendwa wao. Hao walikuwa vijana wa bodaboda  na walikuwa wanasaidia watu kuvuka daraja. Kufikia sasa miili tatu imeopolewa bado mmoja utatafutwa. Sasa wakazi wa eneo hilo wanalalamika kuwa hakuna uhusiano mwema kati yao na wanaojenga barabara inayopita mtaani. Ndio maana wameghadhabika.”

KDI inawatumia baadhi ya wakazi katika vijiji kadhaa vya kibra kupitisha ujumbe wa tahadhari kutokana na hali ya hewa. Hata hivyo Bw. Kipkemboi anasema mara nyingine tukio la ghafla kama mvua iliyonyesha usiku uliotangulia  huwapata wakazi kama bado hajajiandaa. “Tuko na washirika katika mtaa ambao hupokea utabiri wa hali ya hewa kisha wanaiweka katika lugha inayoeleweka na kuwasambazia jamaa na rafiki zao. Lakini wakati wa tukio la ghafla kama hii mara nyingine wakazi huwa hawajajiandaa vilivyo. Nawashauri wakazi wawe makini, ni bora wahamie nyanda za juu kwani sehemu za karibu na mito ni hatari”

Idara ya utabiri wa hali ya hewa awali ilitoa tahadhari kuwa huenda baadhi ya sehemu nchini zikapokea mvua itakayosababisha mafuriko. Idara hiyo iliwataka wananchi kuwa waangalifu kwa kufungua mitaro na kuhamia nyanda za juu kuzuia madhara ya mafuriko. Idara hiyo sasa inasema kuwa huenda mvua ikapunguia kuanzia jumamosi 15, Mei 2021.

Alex Kememwa
+ posts
Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *