Connect with us

Habari

Tekeleza Sheria ya mabadiliko ya Tabia Nchi, Washikadau Wamwambia Rais

Published

on

Gavana Wilber Ottichilo (wa tano kutoka kushoto) Mbunge wa North Horr Chachu Ganya na washikadau wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa wakionyesha nakala za mpango wa kimkakati baada ya mkutano, Nairobi. PICHA: Hisani

Washikadau kutoka mashirika mbalimbali yanayopambana na mabadiliko ya hali ya hewa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuharakisha kutekelezwa kwa sheria ya mabadiliko ya tabia nchi. Mswada wa mabadiliko ya hali ya hewa uliopitishwa kuwa sheria mnamo mwaka 2016, umekosa kutekelezwa kutokana na hatua ya rais  kuchelewa kuunda Baraza la Mabadiliko ya Tabia Nchi inavyoelekeza sheria hiyo.  Mwenyekiti wa kundi la mashirika yanayoangazia mabadiliko ya hali ya hewa John Kioli amesema athari za mabadiliko ya tabia nchi huenda zikaongezeka ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.

“Jiji la Nairobi limekuwa na joto ya juu zaidi ya wastani ya mataifa ya afrika katika siku za hivi majuzi. Hali hii inatuweka katika hali ya hatari zaidi ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa kuzuia athari za sasa na hata zaidi.” Alisema Bw. Kioli

Washikadau hao walikutana Nairobi 20, Julai 2021.

Kati ya wageni mashuhuri katika mkutano huo alikuwa gavana wa kaunti ya Vihiga Wiber Ottichilo aliyemtaka rais awajibike kwa kubuni baraza la kuangazia mabadiliko ya tabia nchi kulingana na sheria.

“Nachukua fursa hii kumsihi rais abuni baraza la kuangazia mabadiliko ya tabia nchi ambalo yeye ni mwenyekiti wake, na ianze kutekeleza majukumu yake kabla ya kongamano kuu la umoja wa mataifa kuhusu hali ya hewa litakalokuwa huko Glascow.” Alisema Bw. Ottichilo.

Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, COP26 UNCCC, litafanyika kuanzia tarehe 1, Novemba 2021 jijini Glascow, Scotland.

Kulingana na sheria hiyo iliyopitishwa na bunge mwaka 2016, The Climate Change Act 2016, rais Kenyatta anatakiwa kubuni Baraza la Kitaifa la Kuangazia Mabadiliko ya Tabia Nchi. Rais atakuwa mwenyekiti wake, naibu wa rais akiwa naibu mwenyekiti na waziri wa mazingira kwa wakati wowote atakuwa katibu wa baraza hilo. Aidha rais atatetua wanachama 9 wa baraza hilo ambao ni pamoja na mawaziri wa fedha, uchumi na wa kawi.

Wengine ni mwenyekiti wa baraza la magavana, wawakilishi wa sekta za kibinafsi, mashirika ya kijamii, jamii ndogondogo na wasomi. Wote watakaoteuliwa kando na maafisa wa serikali watatakiwa kuwa na ufahamu mwema kuhusu masuala ya tabia nchi.

Majukumu ya baraza hilo ni pamoja na kushauri serikali katika ngazi ya kitaifa na magatuzi kuhusu njia mwafaka za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, na kupendekeza sheria madhubuti kutunza mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Alex Kememwa
+ posts
Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *