Connect with us

Habari

Serikali Yaombwa Kuharakisha Juhudi za Ulipaji Fidia kwa Waathiriwa wa Ghasia za Baada ya Uchaguzi

Published

on

 

Mashirika yasiyo ya kiserikali yameiomba serikali kuharakisha mchakato wa ulipaji fidia kwa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa Mwaka wa 2007.

Mratibu mkuu wa muungano wa wahasiriwa wa uchaguzi wa Mwaka wa 2007 Wacira Waheire ameirai serikali ya Kenya Kwanza kutekeleza mapendekezo ya ripoti ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC)  iliyoshinikiza fidia kwa wahasiriwa wa uchaguzi .

Wacira alizungumza jumanne katika eneo la Makina ambapo sherehe ya kimataifa ya haki ya ukweli iliandaliwa

Kwenye Kikao hicho, mhasiriwa mmoja wa uchaguzi wa 2007 alizungumza na kueleza changamoto anazokumbana nazo haswa za kimwili na kisaikolojia.

Alifichua kuwa risasi bado imekwama mwilini mwake na akaiomba serikali kuharakisha fidia .

“Biashara yangu ilianguka kwa sababu ya mapigano. Sijawahi kupata nafuu,” alisema.

Aliongeza kuwa watoto wake hufukuzwa shuleni kwa sababu ya malimbikizo ya karo.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Utu Wetu, Yvonne Oyieke, alikiri changamoto zinazokabili katika kutetea haki na uwajibikaji.

“Kuna haja ya kuendelea kushirikiana ili kuipa serikali shinikizo, hasa kwa kuzingatia hali ya kipekee ya Kenya ya michakato ya uchaguzi,” alisema.

Oyieke aliyataka mashirika ya kiraia na walionusurika kuvumilia hadi haki ipatikane.

Kiongozi wa shirika la Grace Agenda, Jacqueline Mutere lililoko eneo la Kibra alisisitiza umuhimu wa umoja miongoni mwa walionusurika katika unyanyasaji wa kingono baada ya uchaguzi.

“Endeleeni kudai haki ndani ya vikundi na mitandao yenu husika, kwa sababu kuna nguvu katika matendo yenu ya pamoja,” aliwahimiza walionusurika.

Zaidi ya hayo, Mutere alielezea wasiwasi wake kwa kiwewe kinachoendelea kwa waathiriwa na kuangazia hitaji muhimu la huduma za usaidizi wa kisaikolojia na kijamii.

Pia alisisitiza umuhimu wa mipango na programu zinazokuza upatanisho, uponyaji na mshikamano wa kijamii ndani ya jamii zilizogawanyika.

Mutere alitoa wito wa midahalo ya jamii, juhudi za ukumbusho, mageuzi ya kielimu na mipango ya kitamaduni ili kukuza uelewano na umoja.

Mwilwatsi John
+ posts
Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *