Serikali imeonekana kubadilisha mfumo wa kuwataka wakenya kupokea chanjo , kutoka kwenye mfumo wa lazima hadi kwenye mfumo wa kuwashawishi wakenya kupokea chanjo ya COVID -19.
Wakiwa kwenye uzinduzi wa kuhamasisha wananchi kupokea chanjo eneo la Dagoreti hapo jana, mawaziri Fred Matiangi (Usalama wa ndani ) mwenzake wa afya Mutahi kagwe pamoja na Mkurugenzi wa huduma za jiji la nairobi NMS John Mbadi walisisitiza umuhimu wa kila mkenya kupata chanjo ya virusi vya corona .
Waziri Matiangi alisisitiza kuwa wizara ya usalama itashirikiana pamoja na wizara ya afya kuhakikisha wakenya wamepata huduma za kupokea chanjo kwa njia ya upole bila mtu yeyote kushurutishwa.“Mpango wa serikali sasa ni kuhakikisha kwamba tumesaidiana sisi wote .” alisema Waziri Matiangi .
Bw Kagwe aliwataka wakenya kuhakikisha wanachukua jukumu la kibinafs kujikinga dhidi ya virusi vya corona . “Jukumu la kukinga maisha yako ni lako ,jukumu la kukinga familia yako ni lako , jukumu la kukinga Watoto wako ni lako ” alisema waziri kagwe alipokuwa akihutubia umma.
Waziri kagwe pia alitupilia mbali dhana ambazo watu wamekuwa nazo kuhusu chanjo ya virusi vya corona . “Nasikia hadithi nyingi zikisemwa juu ya hii chanjo, wale wengine wanasema eti ukidungwa huwezi kulala , mimi nimedungwa nalala kabisaa.”
Wakaazi wa Nairobi ambao hawajapokea chanjo ya pili walihamasishwa kujitokeza ili kupata chanjo ya pili “ langu ni kuwasihi wale ambao wamepata chanjo ya kwanza kuhakikisha kuwa wamechanjwa kwa mara ya pili. ”