Kundi la wachungaji kwa jina pastrolist parliamentary group na lile la Drylands Learning and Capacity Building pamoja na kanisa la CITAM, yamemezindua mpango maalum wa kuchangisha fedha za kuwanusuru waathiriwa wa njaa.
Akizungumza katika kikao na wanahabari leo kwenye hoteli ya Kiangilikana mjini Nairobi,balozi wa mpango huo maarufu Okoa Maisha ,Ruben kigame, amewarai wakenya na mabalozi wa mataifa mengine kuchanga fedha za kuwanunulia chakula wakaazi wanaokumbwa na baa la njaa katika maeneo kame nchini.
Makundi hayo yamezindua nambari za kutuma mchango maarufu pay bill ambazo ni 188668,akaunti okoa maisha.
‘‘Ikiwa una hata shilingi hamsini,elfu mia moja ama chochote Mungu amekubariki nacho,tuma kupitia nambari hizo na utakuwa umemnunulia mtu ambaye hajala kwa siku kadhaa,na vilevile yule mtoto amabye yuko karibu kutoweka shuleni kwa sababu ya njaa.Najua uchumi ni mbaya ila tusiwe watu wa kujijali tu,tuwajali pia wenzetu ambao wanaumia.’’Alisema Kagame.
Makundi hayo vilevile yamemtaka Rais William Ruto kutangaza Njaa kama janga la kitaifa kutokana na ripoti ya hivi punde ya hali ya ukame Nchini,. Ripoti hiyo inaashiria zaidi ya milioni 4.5 ya wakenya wameathirika na njaa huku wanyama takriban 2.5 wakifariki.
Takwimu hizo pia zinaonesha wanafunzi 54,500 wako kwenye hatari ya kuacha shule huku zikiwa zimesalia siku chache mitihani ya kitaifa kung’oa nanga, kutokana na makali ya njaa.
Ruben kigame ameongeza kwamba wanalenga kunusuru waathiriwa wapatao milioni moja katika mpango huo,akiwaomba wakenya walio na uwezo kuwahifadhi baadhi ya waathiriwa haswa watoto kwa muda.
‘‘Kuna wakenya ambao wana mashamba makubwa na manyumba makubwa,kama inaweza kuyatumia kuhifadhi hata familia mbili pekee,zungumza na viongozi wa maeneo hayo amabayo yameathirika kuchukua zile familia kwa muda tu.Mimi mwenyewe ninaanza kufanya vivyo hivyo leo hii.’’Kigame alirai.
Mbunge wa Laikipia Kaskazini Sara Korere ambaye pia alihudhuria uzinduzi huo,amewarai viongozi,mashirika mbalimbali na wananchi kwa Jumla kusimama na wenzao katika maeneo kame kwa kuchangia vyakula na bidhaa zingine ikizingatiwa zaidi ya watoto 942,000 wameathirika kutokana na utapia mlo.
Wabunge wengine waliohudhuria hafla hiyo kutoka sehemu zinazoathirika na ukame Hususan kaskazini Mashariki mwa Kenya,wameahidi kuhakikisha misaada itakayotolewa itakabidhiwa waathiriwa bila ubaguzi wowote.