Kiongozi wa chama cha ANC Musali Mudavadi amewataka wakenya kufanya uamuzi wa busara pale kura ya maamuzi itakapoandaliwa mwakani
Akizungumza kwenye hafla ya mazishi ya Mzee John Etemesi, katika eneo la Sibanga, eneo bunge la Chereng’any katika kaunti ya Trans Nzoia, Mudavadi amesema huu ni wakati mwafaka wa wakenya kutafakari ni uongozi upi wanatarajia ifikiapo mwaka wa 2022.
Mbunge huyo wa zamani wa Sabatia amesema baadhi ya viongozi waliochaguliwa na wakenya ni wenye ubinafsi mwingi, ujanja na wenye hulka potovu.
Kiongozi huyo wa ANC amewaonya wakenya dhidi ya kupotoshwa na viongozi kama hao wakati kampeni za kura ya maamuzi zitakapoanza.
Mudavadi tayari ameshatangaza azma ya kuwania urais kwenye uchaguzi wa 2022.