Kinara wa Chama cha ANC Musalia Mudavadi amesema pana umuhimu wa wataalam wa masuala ya Sheria na mawakili kuchanganua kwa undani uamuzi wa hapo jana wa mahakama kuhusiana na mchakato mzima wa BBI .
Akizungumza katika eneo bunge la Kilgoris alipokuwa akikutana na wazee na viongozi wa jamii ya Maasai Mudavadi amesema kuwa hitaji la kuweka mbele na bayana matakwa ya wananchi ndilo suala kuu kwenye msukumo wa BBI kwani katiba inawapa nguvu wananchi.
Mudavadi amesisista maamuzi ya taasisi zote ikiwemo mahakama ni vyema kuheshimiwa na wananchi na viongozi.
Kiongozi huyo hata hivyo amekosoa dhana kwamba Rais Uhuru Kenyatta hana nia njema kwenye msukumo wa kuyatetea maslahi ya wananchi.
Mudavadi aliyekutana na wazee hao nyumbani kwake aliyekuwa waziri wa zamani na mbunge Julius Sunkuli, vile vile alitumia fursa hiyo kuwaomba wenyeji wa Kilgoris, kaunti ya Narok na jamii ya Maasai kuunga azma yake mkono ya kuwania urais akiahidi kuyashughulikia maslahi yao kama jamii ya wafugaji.
Mudavadi ameahidi kuzuru maeneo kadhaa ya jamii hiyo na hata kupeleka kampeni zake maeneo mengine ya taifa la Kenya. Anatarajiwa kuzuru kaunti ya Nyeri hapo kesho.