Kituo kipya cha kisasa cha polisi kimezinduliwa hii leo katika eneo bunge la Kibra. Ujenzi wa Kituo hicho ulifadhiliwa na hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge CDF kwa ushirikiano na benki ya KCB pamoja na ile ya Equity. Mradi huo uligharimu shilingi milioni 10 likiwa na jumla ya vyumba 24 ikiwemo afisi na seli.
Akiongea katika hafla ya uzinduzi huo kama mgeni wa heshima, mbunge wa kibra Benard Imran Okoth alisema kituo hicho kinalenga kuimarisha usalama katika mtaa wa Kibra hususan wakati uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia. Okoth hata hivyo amewataka wenyeji kushirikiana na polisi ili kuboresha usalama huku akiwakashifu wenye dhana potovu kwamba kituo kimejengwa kwa ajili ya kuwafunga vijana.
“….huenda kesho ndugu yako ataandikwa hiyo kazi ya polisi.Kwa hivyo usione tunaeka kituo cha polisi hapa ukadhani sisi ni wajinga tunaofanya hiyo kazi.”alisema mbunge Imran.
Imran alisifia kituo hicho akisema kwamba angalau huduma zitapatikana karibu ikilinganishwa na hapo awali ambapo mtu angehitaji kufika kituo cha polisi cha kilimani kutafuta huduma.
“ Nitaongea na waziri Fred Matiangi atuletee Ocpd wetu hapa kibra tusiwe tunaenda hadi kilimani kutafuta Ocpd”Okoth aliongezea.
Miongoni mwa wengine waliofika katika hafla hiyo ni msaidizi wa DCC Teresia Mburu, washikadau katika sekta ya elimu,machifu na manaibu wao ,wakurugenzi wa benki za Equity na KCB kibra, wenyeji miongoni mwa wengine.