Connect with us

Habari

MAJI TAKA YAWAHANGAISHA WAKAZI WA KIBRA

Published

on

Wakaazi wa eneo la Kibra katika kaunti ya Nairobi wanakabiliana na tatizo la maji taka ambalo linawaathiri pakubwa.

Mara si haba, maji taka hufurika katika mitaa na barabara kupelekea hatari kubwa kwa afya ya jamii.
Madhara ya matatizo haya ya maji taka ni ya kutisha.
Wakaazi, haswa watoto, wanakabiliwa na hatari kubwa ya magonjwa kama kipindupindu.
Isitoshe, makazi ya mtaa huu ni magumu kukalika maana kuna harufu mbaya.
Aidha, mazingira yameathirika pia, kwani maji taka yanapofurika husababisha uchafuzi wa mito iliyokaribu na kuchafua maji ambayo yangetumika na wakazi wa Kibra.
Katika kijiji cha Makongeni, wakaazi wamezungumza na kituo cha Pamoja FM na kutueleza kwa kina athari za tatizo hili.
“Mazingira si mazuri, takataka zinajaa kwenye mitaro na maji hayasongi kutokana na uwepo wa taka nyingi, haya yote yanaleta magonjwa, nzi wako hapo, mbu wako hapo, magonjwa madogo madogo tu yanatukumba, Unapata watu wanaendesha na kuumwa na tumbo,” Mwanaisha, mkaazi wa Makongeni alieleza.
Serikali ya kaunti ya Nairobi ilikuwa imewapa vijana kadhaa wa mtaa huu wa Kibra jukumu la kufungua mitaro ya maji taka.
Mwanaisha, ambaye pia ni mmiliki wa nyumba, alithibitisha kwamba kwa kweli wamekuwa wakifungua mitaro ya maji taka na wamewashirikisha katika jukumu hilo.
“Wameshafanya. Wameenda mlango kwa mlango na kuzungumza na kina mama. Walituambia tukusanye taka, tuziweke kando na tuzichome. Kuhusu maji, walituambia tuyamwage kwenye mtaro. Pia wamezungumza na sisi wamiliki wa nyumba na kutuambia tuwaeleze wapangaji wetu kwamba ni lazima taka zichomwe,” Mwanaisha aliongeza.
Franklin Ogeto, mkaazi mwingine wa Makongeni alieleza kwamba maji taka yameathiri vibaya maisha yao kwa njia nyingi, mojawapo ikiwa ni harufu mbaya ambayo mara nyingine haiwezekani kustahimili.
Ogeto pia alisema kwamba watoto wadogo wako katika hatari kubwa ya kuugua kwani wanaweza kugusa uchafu kutoka kwenye maji taka na kisha kugusu chakula.
“Tuna ndugu na dada wadogo. Unapata wanagusa uchafu na kisha kugusa chakula na hii inaweza kuwasababisha kuugua, harufu mbaya pia inatuathiri,” alieleza.
Ogeto alisema kuwa yeye ni miongoni mwa vijana ambao walipewa kazi na serikali ya kaunti ya Nairobi ya kufungua mitaro ya maji taka.
Alisema kwamba kumekuwa na tofauti ikilinganishwa na hapo awali ambapo hali ilikuwa mbaya zaidi.
Aidha, alisema kwamba kaunti ilitoa malipo kwao, lakini walichopata kilikuwa kidogo sana.
“Pesa ambayo inapatikana ni ya sabuni tu, si pesa ambayo inaweza kukusaidia,” Ogeto alinena.
Alimalizia kwa kuambia Pamoja FM kwamba mashirika mengi ya Kibinafsi yamesaidia kwa kutoa vituo vya maji ili watu waweze kunawa mikono.
Listen to TATIZO LA MAJI TAKA.mp3 by Wendy Wangui on #SoundCloud

Wendy Wangui
+ posts
Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *