Zikiwa zimesalia chini ya siku thelathini kabla ya kuanza kwa michuano ya kombe la dunia huko Qatar, shirika la kukabiliana na Ulanguzi wa binadamu (HAART) limeonya huenda visa vya wakenya kusafirishwa nchini humo kinyume cha sheria vikaongezeka siku za hivi karibuni.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kitabu maalum cha kuwasaidia manusura wa ulanguzi wa kibinadamu hapo jana,Mwenyekiti wa shirika hilo Tonny Odera amesema wakenya wengi huenda wakasafirishwa ili kuajiriwa kufanya maandalizi ya mashindano ya kombe la dunia .
Odera amesisitiza kuwa visa vya dhulma dhidi ya wakenya nchini humo vitaongezeka kabla na baada ya michezo hiyo kwani wengi watalazimishwa kufanya kazi wasizokusudia na hata wengine kupelekwa kwa nyumba za watu kufanya kazi kinyume na makubaliano ya kuajiriwa katika maandalizi ya kombe la dunia.
“Utapata kwamba wakenya watakaosafiri sehemu hizo baadhi watakuwa wanapata nafasi za kazi walizotuma maombi zikiwa zimejaa na kulazimishwa kufanya kazi ambazo hawajapokea mafunzo.kwa mfano mtu ataenda huko akitarajia kuwa mlinzi,akifika anaambiwa hizo nafasi zimejaa labda afanye usafi ambao malipo yake yatakuwa ya chini yakilinganishwa na yale ya ulinzi ambao alitarajia kufanya.”Alisema Odera
Odera amehoji kwamba baadhi ya baadhi ya watakaopata nafasi nchini humo watalazimika kutumia hela watakazozipata kulipia vyumba,vyakula na mahitaji mengine ya kimsingi,na kusalia na fedha chache zisiweze kuwarudisha makwao.
Nadeem s. Khan mwenyekiti wa shirika la blue heart internanional aliyehudhuria hafla hiyo,ameitaka serikali kutoa ulinzi wa kutosha kwa mashirika yanayopigana vita dhidi ya ulaguzi wa binadamu ili kupata nguvu zaidi ya kupigania haki za manusura kwani,anadai kesi zingine hushirikisha watu wenye usemi mkubwa hata serikalini ambao huishia kutishia mashirika hayo.
Shirika hilo la HAART hata hivyo linapendekeza maajenti wanaojihusisha na usafirishaji wa watu katika nchi za nje wanapaswa kugharamika endapo wateja wao wataathirika kwa namna yoyote ikiwemo matibabu na hata nauli ya kusafirisha miili ya wafu watakaoripotiwa kutokana na mateso .
HAART Linahimiza serikali kuongeza idadi ya kikosi maalum cha polisi cha kushughulikia maswala ya ulaguzi wa binadamu,kuongezewa maafisa kwani kina maafisa thelathini na saba pekee kote nchini,kikihudumu katika ofisi za Nairobi Mombasa licha ya visa hivyo kukithiri kote nchini.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka shirika hilo,serikali iliwakamata washukiwa kumi na mmoja katika mwaka elfu mbili ishirini ikilinganishwa mwaka wa elfu mbili kumi na tisa ambapo washukiwa arubaini na wanne wa ulaguzi wa binadamu walikatwa,ishara tosha serikali haijapiga hatua kwani visa hivyo vinaripotiwa kwa idadi ya juu .