Vuguvugu la Flone linaloangazia maswala ya wanawake katika Sekta ya uchukuzi hususan matatu,limelamikia kufutwa kazi kiholela na kudhulumiwa kimapenzi kwa wafanyikazi hao .
Mwenyekiti wa shirika la wanawake katika uchukuzi Barani afrika (WIT) chini ya vuguvugu hilo,Elizabeth Njoki Kinuthia,amasema wanawake katika sekta hiyo wanapitia changamoto si haba ikiwemo kufutwa kazi wanapopata uja uzito na vilevile wanapokuwa kwenye siku zao za hedhi.
“Hatuna usalama wa kikazi kwa sababu unapata mwanamke anapoenda kujifungua,kazi yake inaishia pale,anapotaka kurudi kazini anaambiwa atume ombi la kuajiriwa upya.Tena anapoenda katika likizo ya kiujifungua,huwa halipwi.”Njoki alisema.
Njoki vilevile alilalamikia hatua ya baadhi ya wajiri wao wa kiume kuwadhulumu wahudumu hao kimapenzi kwa kutaka kushiriki nao tendo la ndoa kabla ya kuwaajiri kazi.
“Wasimamizi wengi katika sekta ya Uchukuzi ni wanaume na wakati mwingi hawataki kujua kama wewe ni mke wa mtu au mama ya mtu,wanakulazimisha kushiriki mapenzi ili waridhishe haja zao kabla ya kukupa kazi,na ukiwa uko kazini wanakutishia kukufuta kazi. Kesi hizo zinaporipotiwa kwa polisi,hakuna hatua yoyote inachukuliwa kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi,licha kwamba ni vigumu kumnasa mshukiwa kwenye picha anapogusa mwanamke ili iwe ushahidi.”Alifoka Elizabeth
Akizungumza katika kongamano la siku tatu la kila mwaka na ambalo limeng’oa nanga mapema leo jijini Nairobi,Elizabeth aliitaka serikali ya kaunti ya Nairobi kuwajengea wahudumu hao vyoo katikati mwa jiji ili kupata wakati mwafaka wa kujihudumia wanapokuwa katika hali hiyo.
“Gavana wetu Johnson Sakaja tungependa atusaidie kupata mahali pa kujenga vyoo vyetu ili tusaidike tunapokuwa katika hedhi maana tunaumia,kwa sababu unapata wanawake wanakaa barabarani sana bila kubadilisha visodo labda kutokana na umbali wa vyoo,kwa hivyo inabidi wakiwa katika hali hiyo,wachukuwe likizo ambayo hailipiwi,hivyo basi kupata hasara na wakati mwingine hata kufutwa kazi.”Alisema Mwenyekiti huyo.
Baadhi ya Madereva na Utingo kutoka miungano mbalimbali ya matatu ambao pia ni wanachama wa shirika hilo waliohudhuria kongamano hilo, waliunga mkono usemi wa mweneykiti wao wakisema hawana usalama wa kikazi na pia wananyanyaswa na sio tu na waajiri wao bali abiria na maafisa wa polisi na hata wa kaunti.
Sasa wanaitaka serikali kubuni sheria mwafaka ya kuwalinda wanawake katika sekta hiyo,na vilevile kuhakikisha usawa kuzingatia sheria ya theluthi mbili ya kijinsia..
“Itakuwa afueni kama Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi itahakikisha sheria ya theluthi mbili ya kijinsia inakumbatiwa ili wanawake wapate nafasi sawa katika miungano ya matatu hapa Nchini. Na pia serikali itoe amri ya kutofutwa kazi kiholela kwa wanawake katika sekta ya Uchukuzi wanapokwenda kwenye likizo ya kujifungu,inauma ukirejea kazini unapatwa imeekwa mtu mwingine ilihali ulikuwa katika likizo ya kujifungua ambayo hata hukulipwa.”alisema Stamina Bonami Sundays,mmoja wa wanachama hao.
Hata hivyo vuguvugu hilo linaendelea kuelimisha wahudumu hao kuhusu haki zao wanapokuwa kazini na jinsi ya kujiepusha na dhulma,huku likiwahimiza wanawake wasiokuwa na ajira kujiunga na sekta ya Uchukuzi bila uwoga.